Mwanasoka chipukizi Timothy Weah ambaye pia ni mtoto a Rais wa Liberia George Weah, ameitosa rasmi timu ya taifa ya Liberia baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza na timu ya taifa ya Marekani.

Timothy mwenye miaka 18 aliingizwa dakika ya 86 ya mchezo wa kirafiki ambapo timu yake ya Marekani iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Paraguay ambayo imechezwa leo alfajiri nchini Marekani.

Nyota huyo ambaye baba yake alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwaka 1995, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa miaka ya 2000 kuchezea timu hiyo. Timothy amezaliwa February 22, 2000.

Baada ya mchezo Timothy ameeleza furaha yake kwa kusema, ”Hii ndio siku ambayo nilikuwa nikiisubiri kwa hamu katika maisha yangu na leo imetimia, nimefurahi sana na ninashukuru walimu kuniamini na kunipatia nafasi”.

Kinda huyo ambaye hivi karibuni amecheza mechi yake ya kwanza ndani ya PSG pia jana amecheza na kiungo Darlington Nagbe, ambaye ni mtoto wa Joe Nagbe nahodha wa zamani wa Liberia na alicheza sambamba na George Weah.