Wapenda michezo nchini, Jumatano hii usiku walijitokeza kumpokea mwanariadha mashuhuri wa Tanzania John Steven Akhwari katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akhwari alikuwa akitokea Dallas Texas nchini Marekani, ambako alizawadiwa nishani ya ‘TUNU ADIMU’ na Watanzania wanaoishi nchini humo kwa kutambua mchango wake katika michezo.

Wakiwa wametambua ushawishi wa Akhawari kwa wanariadha na wanamichezo kwa ujumla nchini Tanzania,Watanzania wanaoishi Dallas nchini Marekani waliamua kumuenzi kupitia uzalendo na ujasiri wake katika riadha ikiwa ni pamoja na kutambua mchango wake wa zamani na sasa katika mchezo wa riadha kwa Tanzania.

Nishani hiyo ilikabidhiwa kwa Akhwari na Meya wa jiji la Dallas katika maadhimisho ya siku ya Tanzania yaliyofanyika tarehe 28/04/2018 huko Dallas. Aina hiyo ya nishani ilianzishwa kwa ajili ya kutambua mchango wa kipekee wa mtu aliyechangia kwa njia moja ama nyingine jambo Fulani la kipekee kwa Tanzania.

Katika mbio za Marathoni za mwaka 1948 zilizofanyika nchini Mexico, Akhawari alionyesha uhodari na ushujaa wa kipekee uliojawa na uzalendo katika medani za mchezo wa riadha. Hakushinda medali lakini aliweza kuweka rekodi ya kipekee ambayo wanamichezo wengi hawajaweza kuiweka. Pamoja na kupata majeraha na maumivu makali wakati wa mashindano, aliendelea na mbio hadi hatua ya mwishi jambo lililomfanya ajulikane kama ‘baba wa kutokukubali kushindwa’ na kutambulika na vyombo vikubwa vya michezo kama Olympic, FIFA na vinginevyo.

Kwa kutambua Zaidi mchango wake, tunawaletea Mbio za Kimataifa za John Akhwari (JAIM) zilizopewa jina lake kwa kutambua mchango wake. Mbio hizi zitafanyika tarehe 10 Mwezi Juni 2018 jijini Arusha. Zitakuwa ni mbio za aina yake kuwahi kufanyika hapa nchini.

Ungana nasi katika mbio hizi ili kwa pamoja tukumbatie uzalendo wa mwanariadha wetu mstaafu, tuwatambue zaidi waliopo pamoja na kuwatia moyo wanaridha vijana wanaochipukia kuwa Akhwari wa kesho