Bifu la Amigo na Mzee Yusuf lasababisha wawili kutimuliwa Jahazi!

Bifu la waimbaji ‘kiwango’ katika muziki wa taarabu nchini Abubakar Suddy ‘Prince Amigo’ na Mzee Yusuf linaonekana kuzidi kukolea lakini safairi hii ‘likila’ vichwa vya wasanii wawili ambao inadaiwa kuwa karibu na Amigo!

Price Amigo

Taarifa ambazo kipindi cha Mitikisiko ilizipata jana toka kwenye vyanzo vyake vya kuamini vilidai kuwa wasanii Mishi Zele pamoja na Fadhila Mnoga wamewekwa kando kwenye bendi ya First Class inayomilikiwa na Amigo kutokana na wasanii hao kuwa karibu na Amigo!

“Kwasasa bifu la Amigo na Mzee limekuwa kubwa kweli maana hata msanii ukionekana kuwa karibu na Amigo na upo ndani ya bendi ya Jahazi unafukuzwa,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Taarifa hizi zilithibitishwa na Fadhila Mnoga ambaye alizungumza na Mitikisiko na kukiri kuondolewa Jahazi kutokana na ukaribu wake na Amigo.

“Taarifa hizo ni sahihi kabisa lakini siwezi kugombanishwa na Amigo au kusitisha mawasiliano nae eti kwasababu hawaelewani na Mzee siwezi kabisa. Ni kweli sipo kwenye show za jahazi na wala hainishitue nitarudi First Class kwasababu pale ni nyumbani na maisha yatasonga,” alisema Mnoga.

Kwa upande wa Mish Zele alisema kwasasa yupo kwenye ziara ya Jahazi na hajui kitu kinachoendelea Mitandaoni.

Aidha, kwa upande wa Mzee Yusuf alisema Amigo amekuwa akimzungumzia vibaya katika vyombo vya habari lakini kwasababu amerudi kwenye muziki kwa ajili ya kuja kurudisha heshima ya taarabu hawezi kubishana nae.

“Hayo mambo yanayoendelea nayasikia na mengine kuyaona. Nidhamu ndio kila kitu kwangu kama huna nidhamu nakuweka pembeni. Huyo Mnoga na Mish Zele wote wamejulikana kupitia jitihada zangu kama wananikosea adabu kamwe siwezi kuwaangalia. Wote nimewaondoa kwenye bendi,” alisema Mzee Yusuf.

Mapema mwezi uliopita kumekuwa na ‘mipasho’ kupitia mitandao ya kijamii kati ya Mzee Yusuf na Prince Amigo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni baada ya Mzee Yusuf kutaka kumpa ajira kwenye bendi yake ya Jahazi mke wa Amigo, Zireha Husein ‘Boss Lady’ bila kumshirikisha Amigo.

Facebook Comments