Rais Donald Trump na mpinzani wake Joe Biden wanachuana vikali katika uchaguzi wa Rais uliofanyika jana nchini Marekani katika wakati vituo vya kupigia kura vikiendelea kufungwa na matokeo ya kwanza yakiendelea kutolewa.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Trump amepata ushindi kwenye majimbo ya Alabama, Arkansas, Indiana, Kentucky, Mississippi, Oklahoma, Tennessee na West Virginia, ambayo yote alipata pia ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2016.

Mpinzani wake Biden amepata ushindi kwenye jimbo la nyumbani la Delaware, Connecticut, Maryland, Illinois, Massachusetts, Rhode Island, Vermont, Virginia na New Jersey pamoja na wilaya ya mji mkuu, Washington.

Majimbo yote hayo yalikwenda kwa chama cha Democratic wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Hadi sasa Biden anaongoza kwa kura 131 dhidi ya 98 za Trump za Baraza Maalum la Kumchagua Rais na mshindi anahitaji kupata kura 270 miongoni mwa wajumbe 538. Wafuatiliaji wanasema uchaguzi huo utaamuliwa na majimbo yenye ushindani mkali ikiwemo Florida ambalo upande wa Rais Trump umedai kuwa unaelekea kupata ushindi.

Facebook Comments