Rais Donald Trump amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi Mark Esper, na kutangaza kwenye mtandao wa Twitter kwamba afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani “amefutwa”.

Christopher Miller, mkuu wa sasa wa Kituo Cha Kukabiliana na ugaidi amechukua nafasi hiyo mara moja.

Hii ni baada ya wawili hao kutofautiana hadharani katika wiki za hivi karibuni.

Bw. Trump mpaka sasa hajakubali kushindwa katika uchaguzi wa Marekani na Rais mteule Joe Biden, na ameapa kupinga matokeo hayo mahakamani.

Wiki chache zilizosalia kabla ya Biden kuchukua ofisi Januari 20, Trump bado ana uwezo wa kufanya maamuzi.

Bwana Esper alitofautiana na Rais kufuatia mwenendo wa White House kwa majeshi wakati wa maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi mapema mwaka huu.

Wakati Marekani ilipokumbwa na maandamano makubwa kufuatia kifo cha mtu mweusi George Floyd mikononi mwa polisi mjini Minneapolis, Minnesota, mwezi Mei, Bw. Trump alitishia kutumia wanajeshi kuvunja maandamano hayo.

Facebook Comments