Kiongozi wa upinzani na ambaye alikuwa mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema katika uchaguzi wa Oktoba 28 Tundu Lissu ameondoka nchini Tanzania Jumanne (Jana) kuelekea nchini Ubelgiji.

Lissu ambaye alikuwa katika hifadhi ya ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania kwa karibu wiki nzima alianzia safari yake kutokea makazi ya ubalozi kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam.

Kanda ya video inayosambaa inamuonyesha Lissu akitoka makazi ya Balozi wa Ujerumani kwa magari ya ubalozi huku akisindikizwa na maafisa wa ubalozi huo na wa Marekani. Afisa mmoja wa ubalozi alioneoneka akimsindikiza Lissu hadi ndani ya uwanja wa ndege.

Lissu aliomba kinga katika ubalozi wa Ujerumani wiki iliyopita kwa madai kuwa maisha yake yako hatarini. Mwanasiasa huyo ambaye alinusurika jaribio la kuuawa mwaka 2017 alidai kuwa amepata habari za kuaminika kuwa maisha yake yako hatarini.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita polisi nchini Tanzania ilisema haijapata ripoti yoyote ya Lissu kutishiwa maisha.

Baada ya shambulizi la mwaka 2017 Lissu aliishi Ubelgiji kwa miaka karibu mitatu kwa ajili ya matibabu. Alirejea nchini Julai mwaka huu kushiriki katika uchaguzi mkuu na akateuliwa na chama cha Chadema kama mgombea wake urais.

Lissu alifanya kampeni kali dhidi ya Rais Magufuli akimlaumu kwa matumizi mabaya ya fedha za taifa katika miradi ya ujenzi, ukandamizaji wa wapinzani na kumshutumu pia kwa mauaji au kupotea kwa raia kadha wa Tanzania chini ya utawala wake.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini humo, NEC, yalimpa ushindi Rais Magufuli wa asilimia 84 ya kura zote. Chadema na vyama vingine vya upinzani Tanzania mara moja vilipinga matokeo hayo vikidai kulikuwa na ubadhirifu mkubwa na wizi wa kura.

Wapinzani waliitisha maandamano ya amani kupinga matokeo hayo. Serikali mara moja iliwakamata baadhi ya viongozi wa upinzani na wengine kuachiliwa kwa dhamana baadaye.

Mmoja kati ya wapinzani waliokamatwa baada ya uchaguzi Godbless Lema ambaye alikuwa mgombea ubunge wiki hii aliingia nchini Kenya ambako amesema ana nia ya kuomba hifadhi ya kisiasa (bila kutaja katika nchi gani) akidai kuwa amepata vitisho dhidi ya maisha yake.

Msemaji wa serikali ya Tanzania Hassan Abbas amekaririwa na vyombo vya habari akikanusha kwamba kuna vitisho dhidi ya wanasiasa wa upinzani nchini humo.

Chanzo: Sauti ya Amerika, V.O.A

Facebook Comments