Haruna Niyonzima anatarajiwa kuondoka Yanga hivi karibuni, klabu hiyo ya Jangwani imeamua kumpa heshima kubwa ya kumuaga, hakika alistahili.

Naamini licha ya kucheza Simba lakini bado ukiuliza shabiki yeyote wa soka kuwa Niyonzima ni shujaa wa wapi, atakwambia ni wa Yanga, ndiyo ni hivyo kwa kuwa muda mrefu aliodumu klabuni hapo ulimtengenezea ‘chemistry’ kati yake na Wanayanga.

Unamkumbuka Emmanuel Okwi, ndiyo yupo nje ya Tanzania kwa sasa na alishawahi kucheza Yanga, lakini ukiuliza swali lilelile kama la Niyonzima, utapata jibu kubwa Okwi ni wa Simba, sababu ni ileile pia chemistry yake na Wanasimba ni kubwa kuliko alivyokuwa Yanga.

Wawili hao wote ni wachezaji wenye uwezo mkubwa uwanjani na wamefanya makubwa katika soka la Tanzania, lakini utofauti wao ni mmoja tu, walikuwa na jicho tofauti la kuitazama fedha.

Niyonzima alikuwa shujaa ambaye aliamua kudumu muda mrefu Yanga kwa kuwa wakati fulani mambo yalikuwa mazuri kiuchumi na muajiri wake alimwezesha kupata fedha nyingi alizohitaji.

Unakumbuka enzi za Yusuf Manji ndani ya Yanga? Kuna mchezaji gani wa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati angethubutu kuondoka Yanga!

Hata baada ya Manji kuondoka, maisha yakawa magumu, Niyo aliendelea kuvumilia kwa kuwa tayari alishakuwa Mwanayanga, ilipofika hatua mambo yakawa magumu, aliamua kuondoka kwenda Simba, japo wengi tulijua kuwa bado moyo wake upo Yanga.

Okwi kwake aliipenda sana Simba na hata sasa ni shabiki wa Simba, lakini mara zote alikuwa ni mtu ambaye hana utani kwenye suala la fedha.

Mara kadhaa aliondoka na aliporejea thamani yake ilikuwa juu na alirudi kwa dau nono.

Kwa nilivyoona ni kuwa Okwi aliamini kuondoka na kisha kurejea kulikuwa kukiongeza thamani yake na hata umuhimu wake ulikuwa unaonekana mkubwa anaporejea, kwa ufupi alikuwa aki renew thamani yake, wakati Niyonzima aliona fedha alizopata zilimtosha na hakuhitaji ku renew thamani yake.

Yote kwa yote wote ni wachezaji bora, wakati Niyonzima akiondoka Yanga sasa tujiandae kumpokea Okwi mzee wa ku renew thamani ya kiwango chake.

Na John Joseph Haramba, Instagram: @johnharamba

Facebook Comments