Serikali ya Rwanda imetangaza ‘lockdown’ ya siku 10 katika Jiji la Kigali na wilaya nane baada ya kuongezeka visa na vifo vya raia vilivyotokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.

Raia nchini humo wametakiwa kukaa ndani kuanzia Jumamosi Julai 17 hadi Julai 26, 2021 ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Katika masharti hayo biashara, kazi za umma, shule, michezo na burudani zote zimefungwa na idadi ya watu watakaohudhuria mazishi imepunguzwa hadi watu 15 tu.

Watu wanaruhusiwa kutoka nje ya nyumba zao iwapo wanahitaji huduma muhimu au wale ambao wanafanya kazi muhimu zinazohitaji uwepo wao.

Wiki nne zilizopita zimerekodi idadi kubwa ya kesi za maambukizi ambapo karibu wagonjwa 1,000 huripotiwa kwa siku huku siku saba za mwisho zikiwa mbaya zaidi.

Hadi sasa Rwanda imeripoti zaidi ya kesi 50,000 za corona, zaidi ya vifo 600 huku watu 400,000 wakipewa chanjo ya ugonjwa huo.

Facebook Comments